RC. MHITA AAGIZA KITUO CHA AFYA KUANZA KUTOA HUDUMA
Shinyanga MC. Kiongozi Mkuu wa Serikali mkoani Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita ameielekeza Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha Kituo cha Afya cha Ihapa, kilichopo Kata ya Old Shinyanga, kinaanza kutoa huduma mara moja kwa wananchi, kufuatia kukamilika kwa ujenzi na uwekaji wa vifaa tiba.
Mhe. Mhita ametoa agizo hilo Disemba 16, 2025, wakati akizungumza katika kikao kazi na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, ambapo alisisitiza kuwa kuchelewesha utoaji wa huduma katika kituo kilichokamilika ni kuwaumiza wananchi wanaohitaji huduma za afya kwa haraka.
“Ninatoa maelekezo rasmi kwa Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha Kituo cha Afya cha Ihapa kinaanza kazi mara moja. Wakati taratibu za kuongeza watumishi wa afya zikiendelea, huduma zianze sasa kwani vifaa vipo na miundombinu imekamilika,” alisema Mhe. Mhita.
Aidha, RC Mhita amewataka Madiwani kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa halmashauri katika kubuni miradi mipya ya maendeleo na vyanzo vya mapato ya ndani, ili kuiwezesha Manispaa kukua kiuchumi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Katika kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na fursa za kiuchumi, RC Mhita amesisitiza utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kuwawezesha wazawa kupitia mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba kwa vikundi, pamoja na kuwapa zabuni ndogondogo zinazoweza kuinua kipato chao na kuongeza mapato ya Halmashauri.
“Manispaa ya Shinyanga ina vyanzo vingi vya mapato, ni jukumu letu kuhakikisha kila fursa inatumika ipasavyo. Halmashauri ikiwashirikisha wananchi kwa dhati, tutapunguza utegemezi na kuongeza kasi ya maendeleo,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Bw. Peres Kamugisha, amesema amepokea maagizo hayo kwa uzito na kuahidi kushirikiana na timu ya wataalamu pamoja na Baraza la Madiwani kutekeleza kwa haraka ili wananchi waanze kupata huduma katika kituo hicho mapema iwezekanavyo.

Post a Comment