COPRA YANOA MAOFISA UGANI KUINUA KILIMO PWANI
Katibu Tawala Msaidizi , Uchumi na Uzalishaji , Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, amewataka maafisa ugani mkoani humo kuwafikishia wakulima elimu ya mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza ubora wa mazao na ushindani katika masoko ya ndani na nje.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Twamala amesema maafisa ugani wana nafasi kubwa katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi ya kilimo.
Amesisitiza umuhimu wa kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwahamasisha kutumia mbinu bora za uzalishaji, hususan katika mazao ya ufuta na mikunde yanayosimamiwa na mamlaka hiyo.
Aidha, ameishukuru COPRA kwa kusambaza tani sita za mbegu bora za ufuta katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Pwani, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji katika msimu ujao wa kilimo.
Kaimu Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa COPRA, Yona Msaga, ameeleza kuimarika kwa uzalishaji wa ufuta na mikunde kutachangia kuongeza ushindani wa mazao hayo katika masoko ya ndani na nje ya nchi, kuongeza kipato cha wakulima pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Afisa Kilimo wa Kata ya Talawanda, Halmashauri ya Chalinze, Abdallah Almas, amebainisha mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao yenye ubora sambamba na kuboresha huduma za ugani kwa wakulima.
Post a Comment