FCC YAADHIMISHA SIKU YA HAKI YA MLAJI KWA KAMPENI MAALUM
TUME ya Ushindani (FCC) imeanza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki ya Mlaji Duniani kwa kuendesha kampeni maalum ya utoaji elimu kwa walaji na wafanyabiashara, ikiwa ni jitihada za kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao katika soko.
Akizungumza na vyombo Jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwawezesha walaji kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa au huduma, pamoja na kuwahamasisha kuchukua hatua wanapobaini ukiukwaji wa sheria.
Amesema elimu hiyo pia itawalenga wafanyabiashara kwa kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao wa kumlinda mlaji na kuzingatia matakwa ya sheria katika utoaji wa bidhaa na huduma na kuongeza kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu, FCC itatoa elimu kupitia vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii ili kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, FCC itaendesha kliniki za walaji katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Musoma, Njombe na Tanga kwa lengo la kupokea na kushughulikia hoja, malalamiko na changamoto zinazowakabili walaji huku akiwahimiza wananchi wenye changamoto zinazohusiana na bidhaa au huduma kufuatilia vipindi vya elimu vitakavyorushwa na vyombo vya habari, kuhudhuria kliniki za walaji na kutumia fursa hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa ajili ya kupatiwa ufafanuzi au hatua stahiki.
Post a Comment