JESHI LA POLISI LAKAMATA WATUHUMIWA UWINDAJI HARAMU JIJINI MBEYA



Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kufanya oparesheni, misako na doria katika maeneo mbalimbali hali inayopelekea utulivu na amani. Aidha, limeendelea kupata mafanikio katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu na kukamata watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo Mauaji, Unyang’anyi, Uvunjaji, Wizi, Kupatikana na Nyara za Serikali na mengineyo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Zakaria Golani [32] mkazi wa Magigiwe kwa tuhuma za mauaji ya Zengo Somola [27] aliyekuwa mkazi wa Magigiwe kwa kumpiga kwa fimbo kichwani.

 Tukio hilo lilitokea Machi 11, 2026 Kitongoji cha Magigiwe, Kata ya Madibila, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya baada ya mtuhumiwa Zakaria Golani kumfumania Zengo Somola ambaye kwa sasa ni marehemu akimbaka mpwa wake [Jina limehifadhiwa] na kisha kumshambulia kwa kumpiga fimbo kichwani na kupelekea kifo chake.

 Katika muendelezo wa misako hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa Jeshi la Uhifadhi [TANAPA] linawashikilia Amani Lufumba [35] na Hamisi Kisinga [28] wote wakazi wa Sadani Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa kwa tuhuma ya kupatikana na Silaha bunduki bila kibali.

 Watuhumiwa walikamatwa Machi 12, 2026 kufuatia misako na ukaguzi wa nyumba za kulala wageni uliofanyika katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Kijiji na Kata ya Utengule Usangu, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya wakiwa na Silaha Bunduki moja aina ya Rifle yenye namba za usajili 69420 na TZCAR3317 bila kibali.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya linamshikilia Ezekia Kafunja Mwakaboja [70] mkazi wa Kijiji cha Kipande kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha bhangi.

Mtuhumiwa alikamatwa Machi 13, 2026 Kitongoji na Kijiji cha Kipande, Kata ya Kinyala, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya akiwa na shamba linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa robo heka lililopo katika hifadhi ya Msitu wa Mapala likiwa na miche ya dawa za kulevya aina ya bhangi ipatayo 1012.

Miche hiyo ilikatwa na kupimwa uzito na Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mbeya na kupatikana Kilo 318 ambazo ziliharibiwa kwa kuteketezwa moto kwa kibali cha Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe. Taratibu nyingine za kesi mahakamani zinaendelea dhidi yake.

Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari wa Hifadhi ya Wanyama Pori [TAWA] linawashikilia watuhumiwa wawili Sundi Igembe maarufu Luvinza [42] mkazi wa Amazon – Matwiga na George Lufingo maarufu Kalago [68] mkazi wa Kanani – Tunduma Mkoa wa Songwe kwa tuhuma za kupatikana na Meno matatu ya Tembo na kipande kimoja.

Watuhumiwa walikamatwa Machi 15, 2026 huko Ilindi, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Lupa kuelekea Bitimanyanga wakiwa kwenye Pikipiki yenye namba za usajili MC 208 EAY aina ya Boxer. Meno hayo yalikuwa na uzito wa Kilo 11.8. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa ni wawindaji haramu na walikamatwa wakiwa katika haraka za kutafuta wateja/soko.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Ulaya Tamanga [52] na Ella Mpande [42] wote wakazi wa Kalonga nchini Malawi kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.

Watuhumiwa walikamatwa Machi 15, 2026 huko Kijiji cha Makwenje, Kata ya Inyala, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya wakiwa wameingia nchini bila kibali wakiwa na watoto wao wanne wenye umri kati ya miaka 2 hadi 10 kati yao wawili wa kiume na wawli wa kike. Taratibu za kuwakabidhi idara ya uhamiaji zinafanyika.

Wakati huo huo, mnamo Machi 15, 2026 saa 4:45 asubuhi huko eneo la Uyole – Sokoni Jijini Mbeya, Kundi la Wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi waliwazingira watu wanaodaiwa ni wahalifu wanaojihusisha na matukio ya uporaji na upigaji nondo majira ya usiku ambao walikuwa wamejificha ndani ya nyumba moja wapo iliyopo katika eneo hilo.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari wa Kikosi Maalum cha kuzuia na kupambana na matukio ya uhalifu walifika eneo hilo na kukuta kundi la wananchi likiwashambulia watuhumiwa hao kwa kutumia Mawe na Silaha za Jadi.

Katika jitihada za kuwaokoa watuhumiwa hao wananchi walianza kuwarushia mawe Askari Polisi ili kuwazuia wasiweze kuwaokoa wahalifu hao, hata hivyo kutokana na umahiri wa Askari walifanikiwa kuwaokoa jumla ya watuhumiwa 06 kutoka mikononi mwa wananchi na kuwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya kwa matibabu lakini watuhumiwa 04 kati yao walifariki dunia wakipatiwa matibabu ambao ni Erick Nassoro maarufu Erick Madampo [20] mkazi wa Uyole, Meshack Joseph maarufu Skofid [20] mkazi wa Uyole, Abdalah Ngoliyam maarufu Dulla [20] mkazi wa Sakarani na Asajile Isack [25] mkazi wa Sokoni – Kingani.

Aidha, watuhumiwa wengine wawili waliokuwa wamepata majeraha madogo madogo walitibiwa na kuruhusiwa ambao ni Raksi Hamis [23] na Paschal Aron [32] wote wakazi wa Uyole ambao kwa sasa wanashikilia kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tuhuma hizo. 

Katika mahojiano ya awali watuhumiwa walionusulika kuuawa wamekiri kuhusika katika matukio kadhaa ya uhalifu ikiwemo Mauaji, Unyang’anyi wa kutumia Silaha, Uvunjaji na Kujeruhi katika maeneo mbalimbali Jijini Mbeya yakiwemo maeneo ya Isyesye, Iganzo, Hayanga, Manga VETA, Ilomba na Uyole.

Pia, walikutwa na mali mbalimbali walizoiba kwa watu mbalimbali yakiwemo Magodoro, Redio SubWoofer, Televisheni, Mazulia, Mapazia, Majiko ya Gesi na Mitungi yake na mali nyingine za wizi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kufika kituo kikuu cha Polisi Mbeya [Central Police Station] kwa ajili ya utambuzi wa mali zao.

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii. Pia, linatoa wito kwa jamii kulinda rasilimali za Taifa na kuacha kujihusisha na Uwindaji Haramu kwa kuingia ndani ya Hifadhi bila kibali kwani kufanya hivyo ni uhalifu kama uhalifu mwingine na badala yake wafuate taratibu ikiwemo ya umiliki halali wa silaha na kuomba kibali cha kuwinda ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata kwa kutofuata taratibu.





No comments