WAZIRI HOMERA AZINDUA PROGRAMU YA SEMA NA WAZIRI
WANANCHI sasa wana jukwaa la moja kwa moja la kufikisha kero zao serikalini, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Homera kuzindua rasmi programu ya “Sema na Waziri” kupitia kituo cha huduma kwa mteja.
Uzinduzi huo uliofanyika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma,unalenga kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi, huku ukifungua ukurasa mpya wa uwajibikaji na usikivu wa kero za jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Machi 17,2026, Waziri Homera amewahakikishia Watanzania kuwa serikali inaendelea na mchakato wa Katiba mpya, huku akiwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa.
Kauli hiyo imekuja kufuatia simu ya mwananchi kutoka Geita aliyehoji ni lini mchakato huo utaanza rasmi.
Aidha, akizungumzia mafanikio ya kituo hicho, Waziri Homera amesema tangu kuanzishwa kwake Februari 2024, tayari kimepokea jumla ya malalamiko 2,023 kutoka kwa wananchi.
Amesema malalamiko hayo yanahusu masuala nyeti ya kijamii na kiuchumi, yakiwemo ardhi, ndoa na talaka, ajira,huduma ya malezi kwa watoto pamoja na ukatili wa kijinsia ikiashiria mahitaji makubwa ya huduma za kisheria kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba amesema uzinduzi wa programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza matumizi ya teknolojia ili kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi.
Kupitia programu ya “Sema na Waziri”, Waziri atakuwa akizungumza moja kwa moja na wananchi mara mbili hadi tatu kwa mwezi, huku kituo hicho kikiendelea kupokea simu za wananchi kila siku kuanzia asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.
Muda huo unatarajiwa kuongezwa kulingana na mwitikio wa wananchi hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kusikiliza, kutatua changamoto na kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi wao.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Post a Comment