AFRIKA YAPATA MSUKUMO MPYA: SAYANSI NA UBUNIFU VYATAJWA KUWA UFUNGUO WA AFYA IMARA

Afrika imehimizwa kuongeza uwekezaji katika sayansi, utafiti na ubunifu kama njia ya kujenga mifumo imara ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wake. 

Wito huo umetolewa Aprili 7, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani, yakihusisha Wizara ya Afya kwa kushirikiana na World Health Organization (WHO), National Institute for Medical Research (NIMR) pamoja na wadau wa afya akiwemo CHIEB.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kanda wa WHO Afrika, Dkt. Thomas Fedjo amesema bara la Afrika limepiga hatua kubwa katika sekta ya afya, akitaja mafanikio kama maendeleo ya chanjo ya Ebola, uboreshaji wa mifumo ya kugundua mapema magonjwa kama UVIKO-19, pamoja na juhudi za kuanzisha uzalishaji wa chanjo ndani ya bara. 

Amebainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa zikiwemo kuongezeka kwa magonjwa sugu, milipuko mipya ya magonjwa na mifumo dhaifu ya huduma za afya.

Amesisitiza kuwa changamoto hizo haziwezi kushughulikiwa na nchi moja pekee bali zinahitaji ushirikiano mpana kati ya serikali, wataalamu wa afya na jamii kwa ujumla. Aidha, alieleza umuhimu wa mbinu ya “Afya Moja” inayounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira kama njia ya kukabiliana na changamoto za kisasa za kiafya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiufundi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CHIEB, Dkt. Siril Kulaya, amesema kuwa uwekezaji wa sayansi na teknolojia za afya ni msingi wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa haraka na kwa ufanisi. 

Amefafanua kuwa mradi huo unaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kuibua suluhisho bunifu kwa changamoto za kiafya barani Afrika.

Naye Mkurugenzi wa Kukuza na Kuratibu Tafiti kutoka National Institute for Medical Research, Dkt. Nyanda Elias Ntinginya, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika tafiti zinazolenga kukabili magonjwa sugu na milipuko mipya, na kuongeza kuwa ushirikiano na wadau wa kimataifa unasaidia kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika moja kwa moja kuboresha mifumo ya afya na kuleta manufaa kwa jamii.

Taarifa hiyo pia imeinisha kuwa nchi 46 za Afrika tayari zimeandaa mipango ya kitaifa ya usalama wa afya, ikiwa ni pamoja na mikakati ya kukabiliana na usugu wa dawa. Hatua hiyo inalenga sambamba na juhudi za kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Kwa ujumla, World Health Organization inaendelea kusisitiza kuanza kwa enzi mpya ya sekta ya afya barani Afrika inayozingatia usawa wa huduma kwa wote, mifumo imara, matumizi ya teknolojia na umiliki wa ndani wa rasilimali. Mwelekeo huu unatarajiwa kuongeza uwezo wa bara hilo kujitegemea na kuhakikisha ubunifu wa Kiafrika unawanufaisha wananchi wake.

No comments