ENDELEENI KUIMARISHA UHUSIANO NA WALIPAKODI - CG MWENDA
Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchi nzima wametakiwa kuendelea kuimarisha mahusiano na Walipakodi kwa kuwapa elimu ya kodi, kutatua changamoto zao na kuwezesha biashara zao.
Rai hiyo imetolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alipokuwa akizungumza na watumishi wa TRA mkoani Mara kwenye kikao kilichofanyika wilayani Bunda April 14, 2026 ambapo amesema hakuna mamlaka hiyo bila walipakodi hivyo uhusiano nao unapaswa kuimarishwa.
Amesema kuwa wanapaswa kuziona biashara za walipakodi kama biashara zao na kuzithamini kwani TRA ni wabia wa biashara za walipakodi na biashara hizo zinapofanyika vizuri ndiyo kodi inapopatikana.
"Wapatieni wafanyabiashara elimu ya kodi na muende katika maeneo yao na kutatua changamoto zao pamoja na kuwezesha biashara zao, hii itawafanya wajione ni sehemu ya TRA" amesema Bw. Mwenda.
Aidha amewapongeza watumishi wa TRA Mara kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 na kuwataka kuongeza juhudi zaidi katika utendaji kazi wao ili kukamilisha mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kuvuka malengo ya makusanyo yaliyowekwa na Serikali.
Kamishna wa Kodi za ndani Bw. Michael Muhoja amewataka watumishi wa TRA kote nchini kuendelea kutoa elimu ya kodi kutokana na elimu hiyo kutokuwa na mwisho ili kuwawezesha walipakodi wapya na waliopo kuendelea kufuata sheria za kodi.

Post a Comment