MANISPAA KIBAHA YATENGA MILIONI 700 KUKARABATI BARABARA ZILIZOHARIBIKA KWA MVUA


BARAZA la Madiwani Manispaa ya Kibaha limepitisha bajeti ya jumla ya Sh milioni 700 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zilizonyesha kwa muda mrefu.


Fedha hizo zinatokana na mgao wa Sh milioni 50 kwa kila kata katika kata 14 za Manispaa hiyo, utekelezaji wake ukitarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2026/2027.


Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kikanuni cha baraza hilo kilichofanyika katika Manispaa hiyo. 


Akizungumza katika kikao hicho, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Dkt. Mawazo Nicas, amesema awali ilitengwa milioni 420 ambapo kila kata ilikuwa imetengewa Sh milioni 30, lakini kutokana na hali mbaya ya barabara, baraza limeamua kuongeza fedha hizo hadi kufikia Sh milioni 50 kwa kila kata. 


Ameeleza licha ya kuwepo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Manispaa imeona ni vyema kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hiyo kutokana na uharaka wake.


Dkt. Nicas amewapongeza madiwani kwa kuridhia bajeti hiyo,  Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa juhudi za ukusanyaji wa mapato zinazoendelea kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Diwani wa Kata ya Sofu, Mashaka Mahande, ameeleza fedha hizo zitasaidia kurekebisha barabara zilizoharibika zaidi kipindi cha mvua.


Baadhi ya wakazi wa Mailimoja,Tangini, Tumbi akiwemo Emmanuel Charles, Fatuma Issa na Salehe Ally wameishukuru Manispaa kwa uamuzi huo huku wakisisitiza umuhimu wa usimamizi wa utatuzi wa changamoto ya ubovu wa barabara hasa za ndani. 




No comments