MWENYEKITI TUME YA UCHUNGUZI JAJI CHANDE AKANUSHA TUHUMA ZA RIPOTI KUCHAKACHULIWA

 


Mwenyekiti wa Tume ya uchunguzi wa matukio ya vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka 2025, Jaji mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, amekanusha taarifa zinazosambaa kuwa kuongezwa kwa muda wa kazi ya tume kunalenga kuchakachua ripoti yake. 

Kwa mujibu wa Jaji Chande, mchakato huo unaendeshwa kwa uwazi na kwa kuzingatia haki kwa pande zote, huku akibainisha kuwa nyongeza ya siku 21 imeombwa ili kukamilisha kazi kwa ufanisi kutokana na uzito, upana na kina cha uchunguzi huo pamoja na kuchelewa kupokelewa kwa baadhi ya ushahidi muhimu.

Awali tume ilipanga kufanya uchunguzi katika mikoa sita pekee, lakini kutokana na hali halisi ya matukio, ililazimika kupanua wigo hadi kufikia mikoa 12 ili kupata taswira kamili ya kilichojiri. 

Katika uchunguzi huo, Tume hiyo imekuwa ikitafuta majibu ya tofauti za matukio ya vurugu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo sababu za Arusha kushuhudia ghasia kubwa, huku Kilimanjaro ikiwa tulivu, au Zanzibar kubaki shwari wakati Dar es Salaam kukiwa na vurugu licha ya ukaribu wa kijiografia.

No comments