SERIKALI INACHUKUA HATUA ZA HARAKA NA ZA DHARURA KUZUIA MADHARA YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU KWA WANANCHI NA MALI ZAO.



Serikali inaendelea  kuchukua hatua za haraka na za dharura kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo kwenye vijiji vya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu pale yanapojitikeza ili kuokoa maisha ya wananchi na mali zao. 


Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii Mhe. Hamad  Hassan Chande (Mb) katika kikao cha nane cha mkutano wa tatu wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akijibu swali la Mbunge wa Meatu Mhe. Salum Khamis Salum aliyetaka kufahamu mipango ya haraka na ya kudumu kuzuia tembo kuvamia vijiji vya Meatu na kuwarudisha hifadhini.


Mhe. Chande amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kujenga vituo vinne (4) vya Askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na kuviwezesha rasilimali watu pamoja na vitendea kazi muhimu ambapo kupitia vituo hivyo, kati ya mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026 doria zilifanyika na kuwezesha kudhibiti matukio 352 katika Wilaya ya Meatu.


Mhe. Chande ameongeza kuwa, katika kuendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia na mbinu mpya, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi katika mwaka 2026/27 inatarajia kujenga uzio wa umeme (electrified fence) wenye urefu wa kilomita 104 kwenye mpaka wa Pori la Akiba Maswa kwa upande wa magharibi unaopakana na makazi ya wananchi katika Wilaya za Meatu, Itilima na Bariadi ili kudhibiti tembo kutoka nje ya hifadhi na kuingia maeneo ya wananchi

No comments