SERIKALI YAPOKEA MTAMBO WA KISASA KUIMARISHA SEKTA YA UVUVI KIGOMA
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepokea mtambo wa kisasa wa kuzalisha barafu na kukaushia dagaa, pamoja na majokofu yanayotumia nishati ya jua, kutoka mradi wa FISH4ACP ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya mtambo huo iliyofanyika Aprili 14, 2026 katika mwalo wa Katonga mkoani Kigoma, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhe. Hassan Rungwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema kuwa mtambo huo utawasaidia wavuvi kuongeza ufanisi katika shughuli zao na kukuza uzalishaji utakao wawezesha kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Hatua hii itaongeza ubora wa mazao ya uvuvi, kuimarisha ushindani wa bidhaa zetu katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuinua kipato cha wananchi wa Mkoa wa Kigoma,” amesema Mhe. Rungwa.
Aidha, Mhe. Rungwa amewataka wavuvi pamoja na mamlaka zinazosimamia mradi huo kuhakikisha wanatunza mtambo huo na vifaa vyake ili uweze kudumu na kuwanufaisha wananchi pamoja na Serikali kwa ujumla.
Pia Mhe. Rungwa amefafanua kuwa vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mtambo wenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 15 za barafu kwa siku na kukaushia zaidi ya kilo 300 za dagaa kwa siku, majokofu 10 yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita 500 kila moja, pamoja na zaidi ya coolbox 20 zenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita 15 kila moja.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Mhe. Prof. Mohammed Sheikh, amesema uwekezaji huo utachochea ongezeko la thamani ya mazao ya uvuvi na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Aidha, Prof. Sheikh pia amelishukuru Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kupitia mradi wa FISH4ACP kwa kufanikisha upatikanaji wa mtambo huo, na kuwataka wadau wengine kuendelea kuwekeza katika sekta ya uvuvi ili kukuza uzalishaji.
“Ni muhimu kuongeza uwekezaji katika uzalishaji ili kupunguza uhaba wa mazao ya uvuvi na kukidhi mahitaji ya soko,” amesema Prof. Sheikh.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo ikiwemo ujenzi wa bandari za uvuvi katika maeneo ya Bagamoyo na Kilwa, ambazo zitasaidia kurahisisha mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya uvuvi.
Vilevile, Prof. Sheikh amebainisha kuwa mradi wa FISH4ACP ulioanza kutekelezwa nchini mwaka 2020, unalenga kuwawezesha wadau wa sekta ya uvuvi, hususan wanawake, kwa kuwapatia teknolojia na vifaa vinavyoongeza tija katika uzalishaji na uchakataji wa samaki.
Naye Mwakilishi Mkazi wa FAO, Dkt. Nyabenyi Tipo, amesema mradi huo ni wa kipekee barani Afrika, ukiwa na uwezo wa kutumia umeme wa gridi ya taifa pamoja na nishati ya jua, hali inayotarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji wa barafu kwa hadi asilimia 50.
Ameongeza kuwa mfumo huo wa nishati mseto utaongeza ufanisi, kupunguza hasara baada ya uvunaji, na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wavuvi na wasindikaji wa mazao ya uvuvi.





Post a Comment