TANZANIA YAPATA HESHIMA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA JUMUIYA YA MADAKTARI UPASUAJI UBONGO - DKT SAMIA


Nchi yetu imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa kwanza barani Afrika wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) ambao leo nimeufungua jijini Dar es Salaam. Uamuzi huu unadhihirisha imani kubwa katika maendeleo yetu na utayari wetu katika kuimarisha zaidi huduma za afya, hususan huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Matokeo ya kazi kubwa tuliyofanya katika miaka mitano iliyopita katika huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi yanaonekana ambapo;-

1. Hospitali zinazofanya upasuaji wa kibingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zimeongezeka kutoka 2 hadi 7.

2. ⁠Madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wameongezeka kutoka 12 hadi 37.

3. ⁠Tumeongeza kwa kiasi kikubwa vifaa muhimu kama MRI, CT-Scan na X-ray.

Uwekezaji huu umeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache Afrika zenye uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji huo, na sasa inahudumia wagonjwa kutoka nje ya nchi.

Ninashukuru Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania kwa tuzo mliyonipa, hakika, hii ni heshima yetu sote. Serikali yetu itaendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa kuimarisha huduma za afya kwa kuzifanya kuwa bora, nafuu na za uhakika ili kuokoa maisha ya wananchi na kurejesha tumaini kwa jamii.

No comments