WANANCHI WAHIMIZWA KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA UHIFADHI NA KUTUMIA HIFADHI KWA SHUGHULI RAFIKI ZA KIMAZINGIRA
Serikali haitamega eneo la hifadhi ya Msitu wa Loasi ili kuwapatia wananchi kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kutokana na umuhimu wa kiikolojia na kijamii pamoja na kuwa ni chanzo kikuu cha maji ya Mto Loasi na Nsalamba.
Hayo yamesema Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.), wakati akijibu swali la Mhe. Ludoviko Kagele aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kuongeza ardhi kwa wananchi wa Vijiji vya Kasapa, Kingombe, Mlambo, Kala na Ng’undwe kutoka katika Hifadhi ya Lwafi kwa ajili ya kilimo.
“Hii inatokana na ukweli kwamba hifadhi hii ni chanzo kikuu cha maji ya mto Loasi na Nsalamba. Halikadhalika, inahifadhi mimea na wanyama; inasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuepusha migogoro ya wanyama wakali wa waharibifu. Kwa upande mwingine maji yanayotiririka kutoka hifadhi hii huchangia katika maporomoko maarufu ya Kalambo (Kalambo Water Falls) ambayo huchochea utalii na uchumi wa wananchi katika ukanda huo” Amesema Mhe. Chande
Mhe. Chande ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi na kutumia hifadhi kwa shughuli rafiki za kimazingira kama ufugaji nyuki ili kujipatia kipato endelevu.
Awali Mhe. Chande alibainisha kuwa kufikia mwaka 2023 Serikali ilitekeleza Maelekezo ya Baraza la Mawaziri (BLM) kupitia kamati ya mawaziri 8 wa kisekta ya kumega eneo lenye ukubwa wa hekta 10,834 (sawa na ekari 27,050) kutoka kwenye hifadhi hiyo na kugawiwa kwenye vijiji kulingana na mahitaji yao kwa lengo la kupata suluhu ya migogoro iliyotokana na wananchi wanaozunguuka msitu huo kuvamia sehemu ya eneo la hifadhi
Hifadhi ya Msitu Loasi ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 346 la 25/10/ 1957 ikiwa na ukubwa wa hekta 33,468 unazungukwa na vijiji vinne vya King’ombe, Mlambo, Kilambo cha Mkorechi na Mpasa
Post a Comment