PROGRAMU YA MAGEUZI YA MAZINGIRA KUZINDULIWA JUNI 5. 2026
Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2026 jijini Dodoma.
Akizungumza Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Hamad Yussuf Masauni, alisema programu hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uhifadhi wa mazingira kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Masauni amesema mpango huo unakusudia kupanda miti bilioni mbili kila mwaka, kuimarisha biashara ya kaboni, kuongeza matumizi ya nishati safi pamoja na kuanzisha bustani za kijani mijini. Aidha, unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 25,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia sekta za mazingira, taka, misitu na nishati safi.
Ameongeza kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya hekta 469,000 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli zisizo endelevu, huku akisisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi kupunguza ukataji miti na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema jamii ina wajibu wa kushiriki katika utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ili kuhakikisha miji inaendelea kuwa safi na salama kwa kizazi kijacho.








Post a Comment