𝐑𝐂 𝐁𝐀𝐓𝐈𝐋𝐃𝐀 𝐀𝐏𝐎𝐊𝐄𝐀 𝐕𝐘𝐀 𝐑𝐄𝐋𝐈 𝐊𝐔𝐈𝐌𝐀𝐑𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐒𝐇𝐎𝐑𝐎𝐁𝐀 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐒𝐊𝐀𝐙𝐈𝐍𝐈
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kupokea vipande 17,006 vya reli na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya takribani Dola milioni 56 za Marekani.
Amesema, uwekezaji huo utaongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kuchochea biashara na kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Balozi Dkt. Batilda amesema, Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya reli ili kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo na abiria, huku maboresho ya reli ya Kaskazini yakilenga kuongeza kasi ya treni, kubeba mizigo mizito na kuimarisha huduma inayounganisha Bandari ya Tanga na mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo unaenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR) inayolenga kuimarisha mtandao wa reli nchini na kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.
Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amewataka wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya reli, na mali nyingine za umma kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola dhidi ya vitendo vya uharibifu.
Kwa upande wake, Meneja wa TRC Kanda ya Tanga, Christopher Kalisti, amesema reli mpya zitachukua nafasi ya reli za zamani zilizokuwa zikisababisha vizuizi vya mwendo, hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria.
Amesema, kipande kinachoboreshwa kinaunganisha reli ya Kaskazini kutoka Bandari ya Tanga kuelekea Kilimanjaro na Arusha, na reli ya Kati, na kuwa kiungo muhimu cha biashara na usafirishaji.
Naye Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, amesema maboresho ya reli yataongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena zinazoelekea Rwanda, Burundi na nchi nyingine za Afrika Mashariki, hatua itakayoongeza kasi ya utoaji wa mizigo na kuimarisha ushindani wa Bandari ya Tanga.






Post a Comment