STAMICO YAKABIDHIWA LESENI KUBWA YA UTAFITI NA UCHIMBAJI MADINI ADIMU VILIMA VYA WIGU,MOROGORO
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekabidhi Leseni ya Utafiti na Uchimbaji Mkubwa wa Madini Adimu na Muhimu ambayo ni ya kimkakati ya Rare Earth Elements (REE) kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ikiwa ni hatua muhimu ya kuliwezesha shirika kuingia kwenye shughuli za uchimbaji mkubwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote wa Tanzania.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Julai 24, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Sesenga kijiji cha Sesenga Kata ya Mgazi Wilaya ya Morogoro, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuirejesha leseni hiyo kutoka kwa kampuni ya Wigu Hill Mining Company Limited baada ya kumalizika kwa shauri la madai kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji(ICSID).
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni hiyo, Waziri Mavunde amesema kuwa madini ya Rare Earth Elements ni miongoni mwa madini ya kimkakati ambayo kwa sasa yanahitajika kwa kiwango kikubwa duniani kutokana na umuhimu wake katika sekta ya teknolojia ya kisasa.
Pia, Waziri Mavunde amebainisha kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaozunguka mgodi kuuza bidhaa zao mgodini (Local content) na kupitia uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuanza mara moja mchakato wa uendelezaji wa leseni hiyo ili shughuli za uzalishaji madini hayo ziweze kuanza kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amempongeza Waziri Mavunde kwa kuisimamia vizuri Sekta ya Madini na kumuahidi Waziri huyo kuendelea kusimamia sekta hiyo kwa karibu kwa ajili ya masilahi ya taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kuwaamini na kulikabidhi shirika hilo leseni hiyo muhimu na kumhakikishia Waziri Mavunde kuwa STAMICO iko tayari kuanza kazi kwa wakati na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa muda uliopangwa na kwa kuzingatia manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Post a Comment