WAZIRI DKT. GWAJIMA ASAMBARATISHA NDOA YA MWANAFUNZI WA DARASA LA 6 NZEGA

‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameongoza operesheni iliyosambaratisha ndoa ya mwanafunzi wa darasa la sita katika Kata ya Mambali, Nzega mkoani Tabora, kufuatia taarifa alizopokea kupitia ujumbe wa simu kutoka kwa mwananchi mzalendo siku ya Jumapili jioni tarehe 6 Julai, 2025.
‎Taarifa hizo zilibainisha kuwa mtoto huyo ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake, huku familia ikimlazimisha kukubali au endapo atakataa anafukuzwa nyumbani. Dkt. Gwajima alichukua hatua kwa kuziagiza mamlaka za mkoa kushughulikia suala hilo, ambapo mtoto huyo alipatikana tarehe 9 Julai 2025 akiwa huko vijijini na wahusika kukamatwa wamekamatwa kwa hatua za kisheria.
‎ Waziri Gwajima ameeleza kuwa mtoto huyo atarejeshwa shuleni mara moja na kusisitiza kuwa waliohusika lazima wakabiliane na mkono wa sheria, akitahadharisha kuwa Serikali haitavumilia ndoa za utotoni.
‎Aidha, amewaasa wananchi kutumia mawasiliano ya kidigitali kufichua matukio ya ukatili, akiwapongeza wananchi waliojitokeza kutoa taarifa, na kusisitiza kuwa taarifa sasa zinasambaa kwa haraka zaidi, hivyo kila mtu awajibike.
‎ Waziri Gwajima ametoa wito kwa familia  zikizowaingiza watoto kwenye ndoa kuwarudisha shuleni kabla hawajakamatwa, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kesi hizi kupitia kampeni ya (FAECHA) yaani Fahamu, Elimika, Chukua Hatua.

No comments