WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YATIMIZA NDOTO YA RAIS SAMIA.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri,Sera,Bunge na Uratibu,William Lukuvi ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa wa kwanza kutimiza kikamilifu ndoto ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan ya kujenga na kuhamia katika Mji wa Serikali Mtumba.
Waziri Lukuvi ametoa pongezi hizo leo,Julai 23,2025,akiwa katika ziara yake ya kukagua maagizo na utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ya wizara zote kukamilisha ujenzi wa majengo awamu ya pili na kuhamia katika ofisi hizo.
"Majengo haya yamejengwa kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ni wakati wa Rais wa awamu ya tano Hayati Dokta John Magufuli na awamu ya pili ni chini ya Rais Samia ambayo ujenzi wake ni wa ghorofa,niwapongeze kwa kumuheshimisha Rais Samia,mmetekeleza agizo lake kwa vitendo,mmekuwa wa kwanza sio tu kukamilisha jengo bali na kuhamia pia,hongereni sana kwa kutimiza malengo na dhamira yake,
"Niwapongeze pia kwa kutumia samani zilizotengenezwa hapa nchini,nyinyi ndio wasimamizi wa misitu na mmeonyesha mfano mzuri wa kutumia mbao za ndani ya nchi yetu,mmefanya vizuri na kuweni mabalozi wazuri kwa wengine,"amesema.
Awali,Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Dokta Hassan Abbas amesema jengo hilo limegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 20 na kukamilika kwake ni matokeo chanya ya juhudi za Rais Samia katika kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na sekta nzima ya Maliasili na Utalii ili iwanufaishe vyema watanzania.
Mwisho.
Post a Comment