BITEKO AHIMIZA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO VIKAO VYA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewahimiza Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma nchini kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kimkakati yanayofikiwa katika vikao kazi wanavyofanya kwa kutambua kuwa wamebeba dhamana ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia mtaji wa shilingi Trilioni 86 ambao Serikali imewekeza kwenye Taasisi na mashirika yake.

Dkt. Biteko amesema hayo jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs FORUM 2025).

Dkt. Biteko amewahakikishia Watendaji hao kuwa Serikali katika ngazi zote inatambua mchango wa taasisi na mashirika katika ukuaji wa uchumi na pia inatambua mchango wa vikao kazi vya watendaji hao ambavyo vimepelekea mashirika kuongeza mchango wake katika mfuko mkuu wa Taifa.

Amesema uchagiaji wa Shirika la Nyumba la Taifa-NHC, umeongezeka kwa  asilimia 363 katika mfuko mkuu wa Serikali ambapo NHC ilichangia shilingi bilioni 1.2 mwaka 2023/ 24 na mwaka 2024/2025 ilichangia shilingi bilioni 5.5.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka viongozi kufanyia kazi agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango la kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato, huku akimpongeza Msajili wa Hazina kwa kuwa na maono ya kuratibu kikao kazi hicho ili kujadili masuala yatakayosukuma mbele utendaji wa taasisi. 

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema katika kikao kazi hicho kampuni zaidi 300 zimeshiriki huku washiriki wakiwa ni zaidi ya 650.

No comments