DURU YA 4 TUZO YA UANDISHI BUNIFU YAZINDULIWA
Duru la nne la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu mwaka 2025/2026 imezinduliwa leo tarehe 06/08/2025 jijini Dar es salaam ambapo waandishi bunifu nchini wameombwa kujiandaa kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya kushindanishwa.
Akitangaza mbele ya waandishi wa Habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, amesema kuwa ni muda sasa kwa waandishi bunifu nchini kuwawasilisha kazi zao kwa kamati ya Kitaifa ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ili kuweza kuendeleza mazuri yaliyofanywa katika kukuza uandishi na lugha ya Kiswahili nchini.
Pia, Prof.Mkenda amewaeleza waandishi kuwa awali kilifanyika kikao na wadau wa uandishi bunifu kwa ajili ya kuzunguzmia namna ya uboreshaji wa tuzo hizo ili ziendelee kuwa bora na kuleta tija ya uchocheaji wa usomaji vitabu na kukuza lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof Penina Mlama, amesema kuwa miswaada hiyo itahusisha Nyanja ya Riwaya, Ushairi, Hadithi za Watoto na Ushairi kama ilivyokuwa mwaka 2024/2025 na itaanza kupokelewa Agosti 15, mwaka huu hadi Novemba 30. Prof. Mlama amewaomba waandishi bunifu kujitokeza kwa wingi katika kuwasilisha miswaada yao.
Prof.Mlama ameongeza kuwa baada ya zoezi hilo la upokeaji kukamilika majaji wataanza kazi ya kupitia miswada yote na hafla ya kuwatangaza washindi itafanyika tarehe 13/04/2026 ukiwa ni kumbukizi ya kuzaliwa baba wa Taifa, Mwl. Julius Kamabarage Nyerere.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TET,Dkt. Aneth Komba amewashukuru wadau wote wa uandishi ubunifu walioshiriki kikao cha mazungumzo yenye lengo la kuboresha tuzo hiyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau wa uandishi bunifu nchini ambao wameshiriki katika kutoa maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha Tuzo hiyo.
Post a Comment