REA YATOA BILIONI 4.37 KWA JESHI LA KUJENGA TAIFA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Kanali Juma Mrai wakati akifungua mafunzo kwa washiriki toka vikosi 22 vinavyonufaika na mpango wa nishati safi JKT katika bwalo la vijana 834KJ (Makutupora) jijini Dodoma

"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, " Ameongeza Kanali Mrai.

Aidha, ameipongeza REA kwa kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya nishati safi ili kutunza mazingira na kuepuka athari za kiafya zinazohusiana na utegemezi mkubwa wa nishati isiyo kuwa safi

"REA imeiwezesha JKT kwa asilimia 76 Sawa na Shilingi Bilioni 4.37 ya utekelezaji wa nishati safi katika kambi 22 za JKT kwa kuzipatia mashine za kutengeneza mkaa Mbadala 60, majiko banifu 291, mifumo ya gesi ya LPG 180 na masufuria yake, Mkaa Mbadala tani 220, mafunzo kwa vijana 50,000 pamoja na mifumo ya Gesi Vunde 9 " Amesisitiza Kanali Mrai. 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Advera Mwijage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa na askari wa vikosi vilivyopo katika mpango wa REA ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo yao ya kazi.

No comments