UJENZI WA DARAJA LA TAG DARAJANI LAWANUFAISHA WANANCHI WA KATA YA NSALAGA, MBEYA
Kukamilika kwa ujenzi wa daraja la TAG darajani lenye urefu wa mita 9 na upana wa mita 7 linalounganisha jiji la Mbeya na wilaya ya Mbarali lililopo kata ya Nsalaga jijini Mbeya limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwa limerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Fundi Sanifu Mkuu TARURA wilaya ya Mbeya, Bw. Mayungu Mbita amesema kuwa wamepokea fedha shilingi milioni 299 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo baada ya daraja la awali kukatika na mvua.
"Wananchi wa maeneo haya wanajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, mahindi na maharage, kujengwa kwa daraja hili limerahisisha wananchi kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi", amesema.
Naye, mkazi wa mtaa wa Nsalaga, Bw. Alfred Maneno amesema kuwa awali mvua ikinyesha daraja lilikuwa linabomoka mara kwa mara na kusababisha mazingira hatarishi kwakuwa hakukuwa na mawasiliano mazuri ililazimu kuzunguka kwenda barabara ya lami upande wa pili ili kufika mtaa wa Ndundu lakini sasa hivi kumekuwa na mawasiliano mazuri kati ya mtaa wa Ndundu na Nsalaga.
Bi. Mary Mchau mkazi wa mtaa wa Ndundu ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limewatesa kwa muda mrefu hasa wakati wa mvua, walikuwa wanadumbukia kwenye maji wengine walivunjika miguu, watoto walipoteza madaftari ya shule, walishindwa kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi lakini sasa hivi magari makubwa yanapita wanasafirisha mazao yao.
Bw. Edson Gali dereva wa pikipiki mkazi wa Nsalaga amesema kuwa walipata adha kuzunguka kufika mjini mzunguko ulikuwa mkubwa walikuwa wanazunguka na abiria njia haikuwa salama, lakini sasa wanapita bila shida wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo.
Post a Comment