BOT YAONGEZA NGUVU KUSIMAMIA UTULIVU WA UCHUMI NA USALAMA WA MIFUMO YA MALIPO
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kusisitiza majukumu yake ya msingi katika kulinda uthabiti wa uchumi wa nchi kwa kuboresha mifumo ya malipo, kusimamia taasisi za kifedha na kuhakikisha mazingira salama kwa wananchi katika shughuli zao za kifedha.
Aidha, imehimiza wananchi kujenga utamaduni wa kutunza fedha na kuwa na matumizi bora ili kupunguza uwepo wa fedha chafu, hatua itakayosaidia kuepusha gharama kubwa za kuchapisha upya fedha.
Meneja Msaidizi wa Uchumi kutoka BoT, Tawi la Dodoma, Shamy Chamicha, amesema hayo Novemba 19, 2025 wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Benki Kuu na sera mpya ya fedha, katika semina inayowakutanisha waandishi wa habari kutoka Dodoma, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar inayoendelea jijini Dodoma.
Chamicha amebainisha kuwa jukumu kubwa la BoT ni kuandaa, kuchapisha na kutekeleza Sera ya Fedha sambamba na kusimamia mzunguko wa fedha nchini, kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki katika kiwango tulivu.
Ameeleza kupitia sera za fedha, benki hufanya tathmini ya mara kwa mara kuhusu mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki kudhibiti ongezeko au upungufu wa fedha kwenye mzunguko.
Awali akifungua semina hiyo, Meneja wa Idara ya Uendeshaji wa BoT, Tawi la Dodoma, Nolasco Maluli, ameeleza, BoT inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya uchumi, masoko ya fedha na usimamizi wa mifumo ya malipo.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment