DKT. MWIGULU NCHEMBA WAZIRI KUU MPYA TANZANIA, WABUNGE WAMPITISHA, ASUBIRI KUAPISHWA NA RAISI
Wabunge wamemthibitisha
Dokta MWIGULU NCHEMBA, kuwa Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa Kura 369 kati ya Kura 371 zilizopigwa.
Jina hilo lilithibitishwa
kwa kupigiwa Kura baada ya kupendekezwa na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan.
Akitangaza matokeo leo
Bungeni Katibu wa Bunge Baraka Leonard amesema kati ya Kura zilizopigwa, 2
zimeharibika na hakukuwa na Kura ya hapana.
Akisoma wasifu,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari amesema Dokta Nchemba ni Mchumi mbobevu
mwenye Shahada ya Uzamivu katika masuala ya Uchumi.
Amesema Dokta Mwigulu ana
uwezo wa kuchambua na kupima hoja mbalimbali na upeo wake mpana umejidhihirisha
katika utumishi wake wa Umma.
Akifafanua amesema yote
yaliyo katika Dira, Ilani ya CCM na matamanio ya watanzania, yatatimia kama
Taifa litaendelea kuwa na Amani.
Aidha amesema ni lazima maono
ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan na ahadi zitekelezwe.
Pia ametumia nafasi hiyo
kusema Serikali inatambua mahitaji ya watanzania na itaendelea kutatua Kero zao.
Dokta Mwigulu ametumia
nafasi hiyo kukemea Wala Rushwa, Wavivu, Wazembe na kusema watachukuliwa hatua.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan, alipendekeza jina la Dokta
Mwigulu Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi kuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dokta Nchemba anarithi
kiti cha aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Jina la Dokta Nchemba, limeletwa
leo Bungeni na mpambe wa Rais na kutangazwa na Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu.
Dokta Nchemba amewahi
kushika nafasi mbalimbali nchini ikiwemo Naibu Waziri wa Fedha, Waziri wa
Kilimo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Sheria na Katiba na amewahi kuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Bara.
Nafasi ya mwisho
aliyokuwa nayo kabla ya kurudi Bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ni
Waziri wa Fedha.
wakimzungumzia Dokta
Mwigulu baadhi ya Wabunge akiwemo Mbunge wa Mkoani Pemba Profesa Makame Mbarawa,
wamesema Dokta Mwigulu ni wa kipekee.
Naye Mbunge wa Peramiho Jenista
Mhagama amesema Dokta Nchemba ni Jasiri na msimamizi anayetaka mambo yatokee.
Mbunge wa Same Mashariki Anne
Kilango amesema Dokta Mwigulu anafikika huku Mbunge wa Tunduru Kaskazini Ado Shaibu
ameeleza ana imani Dokta Mwigulu atasimamia vizuri katika usimamizi wa Rasilimali
za Taifa katika kuleta Maendeleo.

Post a Comment