RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA SKULI YA SEKONDARI YA AMALI KIZIMKAZI





RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uwekezaji katika miundombinu ya huduma za msingi ni muhimu katika kuchochea ustawi na maendeleo ya wananchi.

Rais Samia amesema hayo mapema leo alipoungana na wakazi wa Mkoa wa Kusini Unguja katika shamrashamra kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi mwaka 2026.

Katika tukio hilo, Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Amali, huku pia akizindua mradi wa maji na kukagua maboresho yanayofanyika katika Kituo cha Afya Kizimkazi.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za msingi zilizo bora, nafuu na za uhakika wakati wote, akieleza kuwa juhudi hizo zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais Samia amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kutunza na kulinda miundombinu inayojengwa, ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Amesema maendeleo ya miundombinu yanahitaji ushirikiano wa Serikali na wananchi, huku akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwa manufaa ya jamii inalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Hatua hizo zimekuja wakati Zanzibar ikiendelea na maandalizi kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi mwaka 2026, ambalo huwakutanisha viongozi, wananchi na wadau mbalimbali katika shughuli za kijamii na maendeleo.



No comments