KWAGILWA AMUAGIZA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE MAALUM MLANDIZI KWA WAKATI

 


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Kwagilwa Reuben, amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi kwa watoto wenye mahitaji maalum Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, kukamilisha ujenzi ifikapo Januari 2026.

Agizo hilo amelitoa Novemba 28, 2025, wakati wa ziara yake ya kazi Mjini Kibaha, ambapo alitembelea shule hiyo na kukutana na watendaji na viongozi mbalimbali .

Amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanaandikisha watoto wao wote waliofikia umri wa kuanza shule za awali na shule za msingi, ikiwemo watoto wenye mahitaji maalum.

Reuben amewaagiza wakurugenzi kuhakikisha ofisi zote za umma zilizo chini ya TAMISEMI zinapimwa na kupatiwa hati.





Vilevile, amekumbusha watumishi wa umma kuzingatia muda wa kazi, akiwataka kuingia saa 1:30 asubuhi na kutoka saa 9:30 jioni, sambamba na kufuata Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009. 

Kadhalika Reuben amewataka viongozi hao kusimamia miradi yote ya Serikali, ikiwemo miradi viporo, ili kuhakikisha inakamilika kabla ya maandalizi ya bajeti ya mwaka 2026. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ,Regina Bieda ameeleza kuwa mradi wa shule hiyo unatekelezwa kupitia fedha za Boost zikiwa milioni 506 ambazo milioni 503 zimeelekezwa kwenye ujenzi na milioni 3 usimamizi.

Naye mkandarasi wa mradi huo, Msafiri Minja, ameeleza walianza ujenzi Novemba 4, 2025, na hadi sasa umefikia asilimia 35, huku akiahidi utakamilika ifikiapo Januari 5, 2026.





No comments