RC MAKALLA AWAHAKIKISHIA USALAMA NA UTULIVU MAAFISA WANAOHUDHURIA MAFUNZO YA NDC
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewakaribisha Wakuu wa Vyombo vya ulinzi na usalama na Maafisa mbalimbali kutoka nchi 16 za Afrika na nje ya Afrika walio kwenye ziara ya mafunzo ya Chuo cha Taifa cha ulinzi (NDC), akiwahakikishia usalama na utulivu kwa kipindi chote cha siku tano watakachokuwa kwenye mafunzo Mkoani Arusha.
CPA Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 10, 2025, alipokuwa akiwakaribisha Maafisa hao 72 ikiwemo kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Afrika Kusini, Malawi pamoja na Bangladesh, ujumbe ukiongozwa na Balozi Meja Jenerali Wilbart Ibuge, Mkuu wa Chuo hicho.
"Mkoa wa Arusha ni Kituo cha Utalii kwa Kanda ya Kaskazini, niwakaribishe sana na mjisikie mpo nyumbani. Arusha inaendelea vyema katika sekta ya utalii na sekta nyinginezo za kiuchumi na imeendelea kuwa salama na tulivu kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya wananchi na Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama." Amesema CPA Makalla.
Katika Programu hiyo ya mafunzo maarufu kama "Tentative Programme for Economy in Tourism", Washiriki hao kutoka nchi 16 wanatarajiwa kutembelea maeneo ya utalii ikiwemo Makao Makuu ya TANAPA, Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha kwa lengo la kujifunza tamaduni na mazingira mbalimbali ya Jiji hilo muhimu kwa uchumi, Utalii na shughuli nyingine za Kidiplomasia.





Post a Comment