WATAALAM WA AFYA MUHIMBILI -MLOGANZILA WATAKIWA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA KWA WAGONJWA.

 


Mkurugenzi msaidizi wa huduma za tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila Dkt. Elineema Meda amewataka wataalam wa afya wa hospitali hiyo kuendelea kuhimiza matumizi sahihi ya dawa kwa wagonjwa pindi wanapowahudumia ili kuepuka usugu wa dawa mwilini.

Dkt. Meda ametoa wito huo katika mdahalo maalum wa kitaaluma uliofanyika hospitalini hapo ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya vimelea sugu dhidi ya dawa ambayo huadhimishwa kuanzia Novemba 18 hadi 24 kila mwaka.

Ameongeza kuwa, Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila ina watalaam maalum kwa ajili ya kusimamia, kushauri , kutoa elimu na kufanya uchunguzi juu ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ili kuepuka changamoto ya dawa kuwa sumu katika mwili wa binadamu.

Katika kuadhimisha wiki hii ya ufahamu wa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa Muhimbili -Mloganzila itakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo mdahalo maalum wa kitaaluma, utoaji wa elimu kwa jamii na huduma ya uchangiaji damu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni chukua hatua sasa, jilinde na kulinda kizazi kijacho juu ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa.









No comments