WAZIRI WA MADINI ANTHONY MAVUNDE AAGIZA TUME YA MADINI KUFUTA LESENI 73 KWA WAMILIKI WALIOSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO.
WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde,ameielekeza Tume ya Madini kufuta jumla ya leseni 73 ambazo wamiliki wake wameshindwa kurekebisha makosa ikiwemo kutozingatia utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki wa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.
Miongoni mwa makosa yanayojitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake wanahodhi maeneo, hawalipi ada stahiki za leseni,hawatekelezi masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye shughuli za madini wala Wajibu wa Makampuni kwa Jamii,wanashindwa kuthibitisha matumizi ya fedha yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika kwenye uendelezaji wa leseni.
Waziri Mavunde ametoa maelekezo hay oleo Jijini Dodoma,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kufuatia uwepo wa makosa hayo, Tume ya Madini ilitoa Hati za Makosa kwa jumla ya leseni 205, ambazo zinajumuisha leseni za utafiti wa madini 110, na leseni za uchimbaji mkubwa na wa kati 95.
Amesema baada ya wamiliki hao wa leseni kupewa hati za makosa, baadhi wamewasilisha utetezi wao na kurekebisha makosa, na baadhi wameshindwa kurekebisha makosa yao wakiwemo wamiliki wa leseni za utafutaji wa madini 44 na wamiliki wa leseni 29 za uchimbaji wa kati wa madini.
Ametoa wito kwa wamiliki wote wa leseni za madini kutekeleza matakwa ya Sheria pamoja na masharti ya leseni wanazozimiliki na kusisitiza kuwa hatawavumilia watu wanaochukua leseni na kukaa nazo bila kuziendeleza.
Moja ya jukumu la Taasisi ya Tume ya Madini iliyo chini ya Wizara ya Madini ni kupokea maombi,kuandaa na kutoa leseni za madini na katika utoaji wa leseni kumekuwa na mwenendo mzuri na idadi ya leseni zinazotolewa kila mwaka wa fedha imeendelea kuongezeka ambapo kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2025,jumla ya leseni 48,673 zimetolewa sawa na asilimia 97.78.

Post a Comment