DTK. PIMA ATANGAZA VITA MIKOPO KAUSHA DAMU
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt.John Pima ameahidi kuzichukulia hatua za kisheria taasisi zote ndogo za kifedha (Micro Finances) zinazotoa huduma katika Manispaa ya Tabora bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Dkt.Pima ametoa rai hii leo Disemba 13,2025 akiongea na watendaji na watumishi wa Tanzania Microfinance Institutions Union (TAMIU) katika ukumbi wa GRANDPENTA HOTEL iliyopo Manispaa ya Tabora katika hafla iliyoandaliwa na umoja huo ya kuuaga mwaka 2025 na kuukaribisha mwaka 2026, aidha hafla ambayo ilitambua jitihada za viongozi waasisi wa umoja huu.
Dkt.Pima ameeleza kuwa, kuna taarifa kwamba kuna taasisi ndogo za kifedha katika Manispaa hii ya Tabora hazijasajiliwa kwa mujibu wa taratibu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za Nchi kutoa huduma kwa taasisi hizi bila kusajiliwa na kutambulika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Business Registrations and Licencing Agency (BRELA), pamoja na kusajiliwa na umoja wa taasisi ndogo za kifedha zinazotoa huduma mathalani TAMIU.
Aidha Dkt.Pima ameongeza kuwa, zipo tasisi zingine zimesajiliwa lakini zinakiuka taratibu za utoaji wa mikopo hii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo ya kausha damu.
Ndugu Pima ametanabaisha kuwa, muda sio mrefu Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi zingine za Serikali itaendesha oparesheni ya kuzitambua taasisi ndogo za kifedha zinazofanya kazi katika Manispaa ya Tabora bila kusajiliwa, aidha zile zinazokiuka masharti ya utoaji mikopo hii, hali inayowaumiza Wananchi na kujikuta wanahangaika.
Kadhalika, Dkt.Pima amewapongeza viongozi wa TAMIU Mkoa wa Tabora kwa kuwa waasisi wa Taasisi hii kubwa na muhimu, ambayo imeasisiwa katika Halmashauri hii ya Tabora kwa mara ya kwanza na hatimae kusambaa Nchi nzima.
Aidha, Dkt.Pima kwa niaba ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ameahidi kuwapa ushirikiana mkubwa taasisi hizi ndogo za kifedha ambazo zimekidhi vigezo vyote katika kuwahudumia watumishi na Wananchi wa Tabora kwa ujumla.

Post a Comment