MAAFISA 28 WA MAGEREZA WAAGWA RASMI BAADA YA KUSTAAFU

Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Desemba 5, 2025 ameongoza hafla maalum ya kuwaaga maafisa na askari 28 waliostaafu kazi baada ya kutumikia Jeshi la Magereza kwa miaka zaidi ya 30. Hafla hiyo imefanyika Uwanja wa Gwaride uliopo Makao Makuu ya Magereza Msalato jijini Dodoma na baadae katika Ukumbi wa Rugimbana.

Walioagwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Kamishna wa Huduma za Urekebu Jeshi la Magereza, CP. Bertha Joseph Minde, pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu pamoja na na askari wa ngazi za chini.

CGP. Katungu amewapongeza wastaafu kwa kulitumikia Taifa kwa weledi, akisisitiza kuwa anatambua mchango wao katika ujenzi wa Jeshi na Taifa kwaujumla, huku akitumia fursa hiyo kuwataka watumishi waliobaki kazini waendelee kufanya kazi kwa bidii huku wakiongeza nidhamu, ushirikiano, umoja na upendo katika kutimiza majukumu, akisisitiza kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo.

 "Tukio hili ni utaratibu na utamaduni wa Jeshi la Magereza kuwaaga maafisa na askari kwa namna hii, ili kutambua mchango wao katika kulitumikia Jeshi la Magereza". alisisitiza CGP. Katungu.

Naye, Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mkurugenzi wautawala na rasilimali watu Bi. Miriam Mbaga, kwa niaba ya uongozi wa Wizara alipongeza uongozi wa Jeshi la Magereza pamoja na watendaji wake kwa kufanya kazi kwa bidii na kudumisha upendo miongoni mwao. 

Akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, CP. Minde aliushukuru uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kuandaa hafla ya kuwaaga, pia alipongeza uongozi kwa kuwezesha matumizi ya Ofisi Mtandao pamoja na kufanikisha matumizi ya nishati safi katika Magereza yote Nchini, akihimiza maafisa na askari wanaobakia kufanya kazi kwa weledi na ushupavu kwa maendeleo ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

No comments