MCHENGERWA ASHIRIKI MKUTANO WA TIBA ASILI INDIA

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, ameshiriki Mkutano wa Pili wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu Tiba Asili uliofanyika New Delhi kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba 2025, ambapo aliikaribisha jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Tanzania katika tafiti, ubunifu, uhamishaji wa teknolojia na biashara ya kimaadili ya tiba asili. 


Mchengerwa alisisitiza mchango wa tiba asili katika kuboresha afya ya jamii na kuendeleza uchumi, akieleza hatua za Tanzania katika kubadilisha tiba asili kutoka mfumo wa jadi kwenda mfumo wa kitaaluma unaotegemea ushahidi wa kisayansi, unaodhibitiwa kisheria na kulindwa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Mkakati wa WHO wa Tiba Asili wa mwaka 2025–2034.


Katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, Tanzania imesajili bidhaa 141 za tiba asili, ambapo zaidi ya asilimia 90 huzalishwa na wazalishaji wadogo wa ndani, hatua inayochangia ajira na ukuaji wa uchumi. 


Serikali inaendelea kuhimiza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kilimo na usindikaji wa mimea tiba, pamoja na upatikanaji wa masoko ya ndani na kimataifa, huku ikilinda haki miliki na maarifa ya jadi kwa kutumia teknolojia za kidijitali na akili mnemba (AI), Mhe. Waziri pia alisaini Hati ya Makubaliano na Wizara ya AYUSH ya India ili kuimarisha ushirikiano katika tiba asili na Ayurveda pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya.

No comments