MHE. MWINJUMA AWASIHI VIJANA WASANII KULINDA AMANI KUPITIA SANAA


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amewataka vijana wasanii nchini kutumia vipaji vyao kulinda na kuimarisha amani kwa njia ya kazi za sanaa zikiwemo muziki, ngoma, filamu, maigizo, uchoraji na fasihi.

Mhe. Mwinjuma ametoa wito huo leo, tarehe 19, Desemba 2025, katika mahafali ya 36 ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), akisisitiza kuwa Sanaa ina nguvu kubwa ya kuelimisha jamii, kupunguza migogoro, kujenga maelewano na kuimarisha uzalendo.
Ameeleza kuwa wasanii wanapaswa kuepuka kutumia sanaa au majukwaa ya mitandao ya kijamii kuchochea chuki, migawanyiko au vurugu, badala yake watumie vipaji vyao kuhubiri amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
“Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha wahitimu, ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana, kwamba amani tuliyonayo nchini mwetu si jambo la kawaida bali ni tunu ya kipekee inayopaswa kulindwa na kuenziwa kila wakati,” amesema Mhe. Mwinjuma.
Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kwa miongo mingi kutokana na busara za viongozi wake na mshikamano wa wananchi, huku akiwataka vijana wasanii kulinda hazina hiyo kwa maneno, matendo na kazi zao za sanaa.

Katika mahafali hayo, Mhe. Mwinjuma ametunuku vyeti kwa wahitimu 234, wakiwemo wahitimu wa Astashahada 107 (wanaume 76 na wanawake 31) na wahitimu wa Stashahada 127 (wanaume 96 na wanawake 31).



TaSUBa ni taasisi ya pekee nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki inayotoa mafunzo ya sanaa katika ngazi za Astashahada na Stashahada.

No comments