TUME YA RAIS KUCHUNGUZA MATUKIO YA OKTOBA 29 YATEMBELEA GEREZA SEGEREA


Tume Huru ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea Siku na baada ya Uchaguzi Oktoba 29, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mohamed Othman Chande, Desemba 11, 2025  imetembelea Gereza la Mahabusu Segerea kwa ajili ya kuzungumza na baadhi ya mahabusu wenye kesi za uhaini.

Ziara hiyo ni sehemu ya majukumu ya tume iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye dhamira ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza baada ya uchaguzi yaliyohusishwa na vurugu za Oktoba 29.

Akiwa gerezani hapo, Jaji Chande alisema tume hiyo ni huru na inafanya kazi kwa uwazi, ikilenga kuwasikiliza watuhumiwa bila woga ili kujua mahitaji yao na namna serikali inaweza kuboresha mifumo ya haki na usimamizi wa sheria.


“Tume hii ni huru, tumekuja kuwasikiliza, muwe huru kuongea,  hakuna atakayemnyooshea mwenzake kidole, kwani Nchi yetu ni ya amani, na tunataka kuendelea kuishi kwa umoja na mshikamano hivyo tuelezane mnataka nini" Alisema Jaji Othman Chande

Uongozi wa gereza uliieleza tume kuwa, hakukuwa na tukio lolote la kifo au madhara kwa binadamu wakati watuhumiwa hao walipokuwa wakipokelewa, na wengi wao tayari wameshatoka baada ya kuachiwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Waliobaki ni wachache wanaoendelea na usikilizwaji wa kesi mahakamani.

Kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Themistocles Ifunya, aliishukuru serikali kwa hatua madhubuti zilizochukuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kuwaachia huru vijana waliokamatwa siku hiyo, hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano magerezani.

No comments