BODI YA WADHAMINI TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD YAZINDULIWA LEO WAZIRI MCHENGERWA AKIKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI YA TAASISI HIYO.
Waziri wa Afya, 𝐌𝐡𝐞. 𝐌𝐨𝐡𝐚𝐦𝐦𝐞𝐝 𝐌𝐜𝐡𝐞𝐧𝐠𝐞𝐫𝐰𝐚 ( 𝐌𝐭𝐮 𝐊𝐚𝐳𝐢 ), leo amezindua rasmi Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) katika hafla iliyofanyika katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mchengerwa alimpongeza Profesa Ephata Kaaya kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ORCI na kusisitiza umuhimu wa Bodi hiyo kusimamia kwa ufanisi majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ili kuhakikisha taasisi inaendelea kutoa huduma bora za uchunguzi na matibabu ya saratani.
Waziri Mchengerwa pia alimpongeza Mkurugenzi wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, pamoja na menejimenti ya taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuboresha huduma za afya na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa alikagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na ORCI, ikiwemo ununuzi na ufungaji wa mashine tatu mpya za kisasa za matibabu ya saratani (LINAC na Cobalt), upatikanaji wa mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu ikiwemo PET CT, uanzishaji wa kinu cha kuzalisha dawa za nuclear (Cyclotron) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya saratani pamoja na ujenzi wa jengo jipya la huduma za kimataifa linalolenga kuimarisha huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Mchengerwa amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za kibingwa na bobezi nchini, kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Serikali itaendelea kuimarisha Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kuwekeza katika miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya saratani ndani ya nchi.
Post a Comment