MEYA KIBAHA ATOA SIKU SABA KWA RASBERY FARM KUDHIBITI KERO YA NZI
BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Madafu, Kata ya Visiga, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wameilalamikia Rasbery Farm, kiwanda cha kufuga kuku, kwa kusababisha kero ya nzi wengi na kuhofia kuhatarisha afya zao na kuathiri shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Wakazi hao akiwemo Sabra Selemani, Hassan Ngwanywama na Mzee Matimbwa, wametoa malalamiko yao kwa Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata hiyo.
Sabra ameomba Kiwanda hicho kiangalie namna ya kuhifadhi taka mbichi zinazotokana na kinyesi cha kuku.
Akizungumza kuhusu kero hiyo, Mtendaji wa Kata ya Visiga, Aloisia Nyello, amesema ofisi yake imekwishapokea malalamiko hayo na wataalamu wa mazingira wamefanya tathmini na kubaini kuwa ni muhimu kupunguza idadi ya kuku kulingana na viwango vinavyotakiwa pamoja na kuongeza matumizi ya dawa za kuua nzi.
Kutokana na hali hiyo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ametoa siku saba kwa uongozi wa Rasbery Farm kuhakikisha wanapuliza dawa maalum za kuua nzi hao ili kuondoa kero na hofu ya athari za kiafya kwa wananchi.
Aidha, amewaagiza maofisa afya na mazingira kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda na kwa wawekezaji ili kutoa maelekezo yanayozingatia sheria za mazingira.
Naye Msimamizi wa Rasbery Farm ameeleza ,wamekuwa wakipuliza madumu mawili ya dawa kila siku na ameahidi ktekeleza maelekezo kabla ya muda wa siku saba uliotolewa.
Post a Comment