SERIKALI KUONGEZA BAJETI YA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI NCHINI


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI imesema itaendelea kuujengea uwezo wa kibajeti Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara za lami kwa awamu kote nchini hatua inayolenga kuboresha miundombinu na kuchochea ukuaji wa uchumi.


Kauli hiyo imetolewa bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu na Naibu Waziri (ELIMU) wa Ofisi hiyo, Mhe. Dkt. Festo Dugange, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Revocatus Chipando, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuongeza mtandao wa barabara za lami kwa kuongeza bajeti.


“Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji hadi mwaka wa fedha 2020/2021 ilikuwa inapokea bajeti ya matengenezo ya barabara na madaraja jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka. Kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka 2025/26 bajeti iliongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 3.2 kwa mwaka,” amesema Dkt. Dugange


Akifafanua hatua zinazochukuliwa, Dkt. Dugange amesema Serikali imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara na madaraja, akitolea mfano Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji ambayo ilipokea shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka 2020/2021 na kuongezeka hadi shilingi bilioni 3.2 kwa mwaka kuanzia 2021/2022 hadi 2025/26.


Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na Benkiy a Dunia kupitia Mradi wa TACTIC (Tier I) inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 9.4, mitaro mikubwa ya maji ya mvua kilomita 5.4, pamoja na Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki Katonga katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji.


Dkt. Dugange amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha uwezo wa TARURA ili iweze kusimamia na kutekeleza ujenzi wa barabara za lami kwa ufanisi zaidi nchini kote, hali itakayorahisisha usafiri na usafirishaji, kuongeza fursa za biashara na kuboresha maisha ya wananchi.




No comments