PWANI YAENDELEA KUZALISHA AJIRA KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa vitendo, hususan uzalishaji wa ajira kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kunenge ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea kongani ya viwanda ya Gaini Company Limited iliyopo Kata ya Kikongo, wilayani Kibaha mkoani Pwani, mradi unaotarajiwa kuzalisha ajira zipatazo 1,500 ifikapo Machi 2026.
Ameeleza uwekezaji huo unaendana na mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii .
Amesema Mkoa unashirikiana na taasisi wezeshi zikiwemo TANESCO, DAWASA na TANROADS ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki na yasiyo na urasimu.
Vilevile Kunenge amefafanua, mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze umefanyiwa upembuzi yakinifu wa shilingi bilioni 2.3 na TPDC, hatua itakayoongeza upatikanaji wa nishati kwa viwanda mkoani humo.
Nae Meneja wa Mradi wa kongani hiyo, QS Bradley Cuthbert Muro, amesema ujenzi wa viwanda viwili umefikia hatua za mwisho na uzalishaji unatarajiwa kuanza Machi mwaka huu.
Post a Comment