TUME YA MADINI YATUMIA MAONYESHO YA 12 YA BIASHARA YA KIMATAIFA ZANZIBAR KUTOA ELIMU KWA WANANCHI.

Tume ya Madini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar,kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna wanavyoweza kushiriki moja kwa moja katika mnyororo wa thamani wa madini na kunufaika kiuchumi.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, amesema maonyesho hayo yanafanyika katika eneo la Fumba, Zanzibar.

“Sekta ya madini si kwa wawekezaji wakubwa pekee. Kuna fursa nyingi kwa wachimbaji wadogo, wajasiriamali, vijana na wanawake kushiriki kupitia uchimbaji mdogo, uchenjuaji, biashara ya madini, pamoja na utoaji wa bidhaa na huduma kwenye migodi,” amesema Mwase.
Ameongeza kuwa Tume inawahamasisha wananchi kuomba Leseni za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PMLs), kuanzisha viwanda vidogo vya kukata na kung’arisha madini (lapidaries), pamoja na shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu, vito vya thamani na madini ya viwandani ili kuongeza thamani kabla ya kuyapeleka sokoni.

Aidha, Mwase amesisitiza umuhimu wa kutumia masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini, ambavyo huwezesha wachimbaji na wafanyabiashara kuuza madini yao kwa uwazi na kwa kuzingatia bei elekezi za kila siku zinazotolewa na Tume kulingana na mwenendo wa Soko la Dunia.
Kuhusu ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma kwenye migodi, amesema Tume inatekeleza kikamilifu Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, zinazolenga kuhamasisha ajira kwa Watanzania, ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani, pamoja na uhamishaji wa ujuzi na teknolojia.

“Huduma za upishi, usafirishaji, usambazaji wa mafuta, ujenzi, ulinzi na nyinginezo ni fursa kubwa kwa Watanzania. Tunawahimiza wasajili biashara zao, wapate vibali vinavyotakiwa na waongeze uwezo wao wa kiufundi ili kunufaika zaidi,” ameeleza.

Amebainisha pia kuwa vijana wa Kitanzania wanayo nafasi kubwa ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya madini, hususan wenye taaluma za sayansi, uhandisi, mazingira, uhasibu, mawasiliano na uendeshaji wa mitambo.
Maonesho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kujenga Ukuaji Jumuishi Kupitia Biashara na Ubunifu,” ambapo Tume ya Madini imeweka mkazo katika kuonesha fursa za utafiti wa madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini, pamoja na utoaji wa huduma na bidhaa kwenye migodi.

Maonesho ya hayo yataendelea hadi tarehe 16 Januari, 2026, ambapo wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Tume ya Madini ili kupata elimu, machapisho ya taarifa na kubaini fursa mbalimbali za uwekezaji na kushiriki katika sekta ya madini inayokua kwa kasi nchini Tanzania.

No comments