BILIONI 68.7 KUWA CHACHU YA MAENDELEO KWA WANANCHI MANISPAA KIBAHA


Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani wamepitisha kwa kishindo bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya sh Bilioni 68.7 katika Baraza Maalum la Madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Kibaha.

Akizungumza wakati wa kupitisha bajeti hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amesema bajeti hiyo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi na imezingatia mahitaji halisi ya Halmashauri.

Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Kibaha, Aziza Mruma, amesema Halmashauri imekisia kutumia kiasi hicho cha sh Bilioni 68.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia sita ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2025/2026.

Kwa mujibu wa Mruma, katika mchanganuo wa bajeti hiyo, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa sh Bilioni 17.8, miradi ya maendeleo Shilingi Bilioni 8.7, huku asilimia 60 ya mapato ya ndani ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 40 kwenye matumizi ya kawaida.

Vilevile, sh Bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Katika mwaka huo wa fedha, Halmashauri inatarajia kujenga kituo kimoja cha afya na zahanati mbili, pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Bilioni 1.3.







No comments