MAKONDA AKERWA NA SIFA ZA WAAMUZI KUPEWA WAGENI, BODI YA LIGI WAMEPWA RUNGU



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameitaka Bodi ya Ligi na wadau wa soka nchini kuongeza umakini katika usimamizi wa waamuzi, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu wa kuhakikisha michezo inachezwa kwa haki na ufanisi.

Akizungumza leo Aprili 30, 2026, katika mkutano na wadau wa sekta ya habari uliofanyika jijini Arusha, Makonda alisema hakufurahishwa na hali ya Watanzania kumpongeza mwamuzi kutoka Kenya, jambo alilodai linaashiria uwepo wa changamoto kwa waamuzi wa ndani.

Alieleza kuwa wizara yake ina jukumu la kulea na kusimamia sekta bila kuingilia moja kwa moja maamuzi ya kiutendaji, hivyo akaitaka Bodi ya Ligi kushirikiana na wataalamu wa upangaji wa waamuzi kuhakikisha wanazingatia maadili na weledi katika kazi zao.

Makonda alionya kuwa waamuzi wasipodhibitiwa wanaweza kuwa chanzo cha malalamiko na kuharibu taswira ya michezo nchini, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuona “fair game” inatawala katika mashindano yote ya soka Tanzania.

Aidha, alimtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha kunakuwa na mazungumzo kati ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kushughulikia malalamiko ya muda mrefu kuhusu waamuzi. Kauli hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani yaliyofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Arusha.















No comments