MUHIMBILI- MLOGANZILA IMEENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA UCHUJAJI DAMU KWA WAGONJWA WA FIGO



Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila yaendelea kuboresha huduma za uchujaji damu kwa wagonjwa wenye
changamoto ya figo kwa lengo la kuongeza usalama na ufanisi wa matibabu.

Akizungumza katika Mdahalo wa kitaaluma(Symposium), Daktari Bingwa Bobezi wa upandikizaji figo kutoka Korea Kusini, Prof. Park, Kwan Tae, ameeleza kuwa hospitali imehamasisha utengenezaji wa AVF (Arterio Venous Fistula) kama njia bora na salama zaidi kwa wagonjwa wanaohitaji uchujaji wa damu. Wagonjwa waliowekewa AVF wanaweza kuchuja damu kwa ufanisi zaidi bila kuwa na catheter mwilini mwao, jambo ambalo limepunguza hatari ya maambukizi na kuboresha ubora wa maisha yao.

Amefafanua kuwa wagonjwa wengi wamekuwa wakitumia catheter kwa ajili ya kuchuja damu, wakati kitaalamu zinapaswa kutumika kwa muda mfupi wa wiki mbili hadi mwezi mmoja, na kwa catheter za kudumu zinatumika hadi mwaka mmoja.

Aidha, amesisitiza kuwa upandikizaji figo umekuwa suluhisho la kudumu kwa wagonjwa wa figo, badala ya kundelea kutegemea mashine za kuchuja damu maisha yote. Hivyo amehimiza ndugu wa wagonjwa kujitolea kuchangia figo, akieleza kuwa uvunaji figo hufanyika kwa upasuaji wa matundu madogo ambao haumwachi mchangiaji alama kubwa na humwezesha kuendelea kuishi maisha ya kawaida akiwa na figo moja.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeendelea kuwahimiza wagonjwa wote wenye changamoto ya figo kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwekewa njia ya kudumu ya kuchuja damu wanapokuwa wakisubiri kupandikizwa figo, huku ikiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchangiaji figo katika kuokoa maisha.






No comments