TRA UNITED YAHAMIA RASMI MKOA WA ARUSHA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumatano Februari 25, 2026 kwenye Makao Makuu ya Mamlaka ya Mapato TRA, Mkoa wa Arusha ameipokea rasmi timu ya Mpira wa Miguu ya TRA United, inayoshiriki Ligi Kuu na ambayo imehamishia makazi yake Mkoani Arusha, akiwaomba wananchi kuiunga Mkono timu hiyo.

Wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Makalla akiutaja Mkoa wa Arusha kama Mkoa wa Utalii na Jiji la biashara, amesema kwasasa kutakuwa na Timu mbili zinazoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara,  ikiwa ni sehemu ya hamasa kuelekea kwenye michuano mikubwa zaidi ya Mpira wa miguu Barani Afrika (AFCON 2027) ambapo baadhi ya michezo yake itachezwa Mkoani Arusha.

"Nawakaribisha rasmi Mkoa wa Arusha na mmekuja sehemu sahihi kwani nguvu kubwa aliyonayo Rais Samia katika kuwaletea maendeleo wananchi imetokana na moyo wa wa uzalendo wa wananchi wa Arusha na jukumu walilonalo TRA, ninyi mkiwa mabalozi wao katika kutimiza majukumu yao na niwaahidi mkiwa hapa tutawaimarisha zaidi kwa kuwapa nguvu ya mashabiki na kila aina ya sapoti ili mfanye vizuri na ujio wenu hapa ni mkakati wa hamasa kuelekea AFCON 2027." Amesema Mhe. Makalla.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa wa Arusha Bw. Mathew Ruangisa na Msemaji wa Klabu hiyo Bi. Christina Mwagala, wamemshukuru Mhe. Makalla na wananchi wa Mkoa wa Arusha  kwa mapokezi yao, wakieleza matarajio ya timu hiyo kufanya vizuri zaidi katika michezo yake ya ligi kuu pamoja na kuitangaza Arusha katika kipindi chote watakachokuwa Mkoani hapa.

No comments