CCM YARIDHISHWA NA BANDARI KAVU ISAKA


 Chama Cha Mapinduzi, kimeridhishwa na mradi wa Bandari Kavu ya Isaka, iliyopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni-10.

Akikagua mradi huo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, ametoa wito kwa wananchi walio karibu na eneo la mradi kulinda miundombinu, huku akisema kutokuilinda ni sawa na kuihujumu Isaka na nchi nzima kwa ujumla.

Baadhi ya faida za mradi huo ni kusaidia urahisishaji wa usafirishaji wa mizigo kwa nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda na Burundi.

Aidha, Mwenezi Kihongosi amesema shughuli hizo zitafanyika katika bandari kavu ya Isaka tofauti na awali, ambapo ililazimu shughuli kufanyika katika bandari ya Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, ameutaka uongozi wa bandari pamoja na Mbunge wa Jimbo la Msalala, Johnson Magangila, kuhakikisha mradi huo unatoa kipaumbele kwa wazawa wa maeneo hayo, ambao ni wakazi wa Isaka na Kahama.

Kihongosi yupo ziarani mkoani Shinyanga, ambayo pia itamfikisha katika mikoa ya Simiyu, Mwanza na Geita, na katika ziara hiyo, anashiriki shughuli mbalimbali ikiwemo ukaguzi wa miradi ya maendeleo.



No comments