HALMASHAURI YA MAFIA YAPITISHA BAJETI YA BILIONI 25.7, DC ASISITIZA UKUSANYAJI MADHUBITI WA MAPATO


Baraza la Madiwani la Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani, limepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye jumla ya Shilingi Bilioni 25.7, huku likisisitiza utekelezaji wa kitaalamu na ukusanyaji zaidi wa mapato.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Gulam Mohammed, akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Chicco, amesema kipaumbele kitawekwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na masuala ya msingi kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, ameitaka Halmashauri kuwa na timu yenye weledi na uzalendo itakayosaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuibua vyanzo vipya ili wilaya ipige hatua kiuchumi.

Vilevile ameeleza bajeti hiyo itasaidia kupunguza kero za watumishi kwa kulipa madeni ya stahiki zao na kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo madarasa, vituo vya afya na upatikanaji wa madawati.

Awali akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu, Deusdedith Joseph, amefafanua kuwa bajeti ya mwaka 2026/2027 imeongezeka kwa asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2025/2026.

Kati ya fedha hizo, Bilioni 3.1 zinatarajiwa kukusanywa kutoka mapato ya ndani,  Bilioni nane zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku sh. Milioni 313.8 zikitengwa kwa utoaji wa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Madiwani wameahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa bajeti hiyo kwa kuzingatia maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


No comments