MGALU AGUSA MISIKITI NA SHULE BAGAMOYO, NA KUHAMASISHA MALEZI BORA

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, CPA Subira Khamis Mgalu, ameendelea kuunga mkono jamii kwa vitendo kupitia matukio ya kijamii na kielimu, huku akisisitiza mshikamano na maadili.

Katika kuuenzi Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kipindi cha Kwaresma, amegawa futari katika misikiti saba, vituo vinne vya watoto yatima, shule tano pamoja na Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bagamoyo, hatua iliyolenga kugusa makundi maalum na kuimarisha upendo na umoja miongoni mwa wananchi.

Futari hiyo imewafikia wanafunzi wa Shule za Sekondari Bagamoyo, Mapinga, Dunda, Matimbwa na Kingani; watoto wanaolelewa katika vituo vya Amani Zinga, Kwa Masister Makurunge, Moyo Mmoja Dunda na Al Rayan  na waumini katika misikiti mbalimbali wilayani humo.

Wakati huo huo, Mgalu ameshiriki mashindano ya Qur’an yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Wilaya ya Bagamoyo, ambapo wito kwa wazazi kuendelea kuweka kipaumbele katika malezi bora, maadili mema na elimu kwa watoto, akisisitiza kuwa msingi wa taifa imara unaanzia katika ngazi ya familia.

Aidha katika kuimarisha sekta ya elimu,  Mgalu alichangia sh. 500,000 kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya photocopy katika Shule ya Sekondari Mapinga.

Amegawa futari kwa wanafunzi wanaokaa kambini na kuahidi kushughulikia upatikanaji wa kompyuta ili kurahisisha kazi za walimu na kuinua kiwango cha taaluma .

Matukio hayo yamefanyika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kuadhimishwa tarehe 8 Machi 2026, huku ngazi ya wilaya yakifanyika Machi 5, 2026 wilayani Bagamoyo.

No comments