MANISPAA YA KIBAHA YANUNUA MAGARI 7, YALENGA KUONGEZA UFANISI NA UKUSANYAJI MAPATO
Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imenunua magari saba yenye thamani ya Sh bilioni 1.356 kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Ununuzi wa magari hayo umepitishwa na Baraza la Madiwani kupitia bajeti hiyo, ambapo yanatarajiwa kutumika katika idara mbalimbali za halmashauri .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema ununuzi huo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa wakati.
Ameongeza kuwa hadi sasa halmashauri imepokea magari matatu kati ya saba yaliyopangwa kununuliwa, huku yaliyobaki yakitarajiwa kuwasili hivi karibuni.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ameipongeza menejimenti ya halmashauri hiyo kwa mafanikio ya ukusanyaji wa mapato, akieleza kuwa Manispaa hiyo imeshika nafasi ya pili kati ya halmashauri 184 nchini.
Mkuu wa Idara ya Utumishi na Rasilimali Watu, Mrisho Mlele, amefafanua ununuzi wa magari hayo utasaidia kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo na kushughulikia kero za wananchi.
Post a Comment