OSHA YAIPONGEZA TASAC KWA KUTOA MAFUNZO YA USALAMA NA AFYA MAHALA PA KAZI
Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) umelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa juhudi zake za kuhakikisha watumishi wake wanapatiwa mafunzo ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi mara kwa mara, hatua inayochangia kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa watumishi wa TASAC leo, tarehe 9 Machi 2026 jijini Dar es Salaam, Mwezeshaji kutoka OSHA, Bw. Saimon Lwaho, amesema hatua ya shirika hilo kuendelea kuomba na kuratibu mafunzo kutoka OSHA inaonesha namna Menejimenti ya TASAC inavyotekeleza kikamilifu matakwa ya sheria.
Ameeleza kuwa TASAC imekuwa mfano mzuri wa utekelezaji wa Kifungu cha 34 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi, kinachomtaka mwajiri kuhakikisha watumishi wake wanapatiwa mafunzo ya usalama na afya ili wawe na uelewa sahihi wa namna ya kujikinga na hatari zinazoweza kujitokeza wanapokuwa kazini.
“Naishukuru na kuipongeza Menejimenti ya TASAC kwa kukitendea haki Kifungu cha 34 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kinachomtaka mwajiri kuhakikisha watumishi wanapatiwa mafunzo ili wawe na uelewa wa kutosha wa masuala ya usalama na afya wanapokuwa kazini,” amesema Bw. Lwaho.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi TASAC, Bi. Selina Mokiti, amesema mafunzo hayo ni ya lazima kwa kila mtumishi, ndiyo maana kamati hiyo imekuwa ikiandaa mafunzo hayo kila mwaka ili kuongeza uelewa na kuimarisha utamaduni wa usalama kazini.
Ameongeza kuwa mafunzo ya mwaka huu yamewahusisha watumishi wapya pamoja na wale waliokuwepo kazini kwa muda mrefu, ambapo jumla ya watumishi takribani 43 kutoka Makao Makuu na ofisi za mikoani wameshiriki mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea watumishi uwezo wa kutambua na kudhibiti hatari zinazoweza kujitokeza mahala pa kazi, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa kanuni na taratibu za usalama na afya kazini ndani ya shirika.

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)


Post a Comment