RAIS SAMIA APOKEA TAARIFA YA TUME KUHUSU TAHMINI YA MIGOGORO YA ARDHI NA UHAMAJI NGORONGORO
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Machi 12, 2026 amepokea rasmi taarifa ya Tume ya Kutathmini Migogoro ya Ardhi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na tathmini ya utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Dkt. Samia amesema eneo la Ngorongoro ni rasilimali muhimu inayopaswa kulindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ambapo ameeleza kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa bioanuai, utalii pamoja na historia ya mwanzo wa mwanadamu duniani, hivyo hatua zozote zinazochukuliwa zinapaswa kuzingatia maslahi ya taifa na jamii zinazozunguka eneo hilo.
Rais Samia pia amesisitiza kuwa Serikali ina jukumu la kulinda mfumo wa ikolojia unaounganisha Hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya jirani kama Loliondo pamoja na Lake Natron na kuwa utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari unalenga kulinda mazingira ya eneo la hifadhi na kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinaendelea bila kuathiri maisha ya wananchi.
Aidha, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha utekelezaji wa zoezi hilo kwa kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika awamu za mwanzo. Hatua hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ardhi na kuhakikisha ustawi wa wananchi wanaohama pamoja na kulinda mazingira ya asili ya eneo la hifadhi.
Kwa mujibu wa taarifa ya tume hiyo, ongezeko la watu, mifugo na makazi ndani ya eneo la hifadhi limeongeza shinikizo kubwa katika matumizi ya ardhi na rasilimali za mazingira hali hiyo imesababisha changamoto za kimazingira na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, jambo ambalo linahitaji hatua madhubuti ili kulinda urithi wa asili wa taifa.


.jpeg)
Post a Comment