SERIKALI YAIMARISHA ULINZI DHIDI YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA MAENEO YA MIPAKANI


Serikali kupitia Wizara ya Afya chini ya Idara ya Kinga, Kitengo cha Afya Mazingira sehemu ya Huduma za Afya Mipakani kwa kushirikiana na Shirika la Afya Dunia (WHO) imeendelea  kuimarisha ulinzi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza katika maeneo ya mipakani, kufuatia uchambuzi wa kina wa takwimu kuhusu mienendo ya watu wanaovuka mipaka isiyo rasmi katika mikoa ya Kigoma na Rukwa.


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa huduma za Afya mipakani Dkt. Remidius Kakulu katika kikao kazi cha siku tano kinachofanyika  mkoani Morogoro, amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoweza kuingia nchini kupitia njia zisizo rasmi za mipakani.


“Wataalamu wa udhibiti wa magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Chuo Kikuu cha Ardhi wanapitia na kuchambua kwa kina taarifa zilizokusanywa na Wizara ya Afya kutoka maeneo mbalimbali ya mipakani, ili kubaini mwenendo wa usafiri wa watu, njia zinazotumika mara kwa mara, maeneo yanayotembelewa mara nyingi na wageni kutoka nje pamoja na changamoto zinazoweza kuongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.”amesema Dkt.Kakulu


Naye,Mratibu wa masuala ya Ujirani mwema Bw. Athanas Lucas amesema taarifa hii ni muhimu katika kuimarisha udhibiti wa mgonjwa kwa kushirikiana na nchi tunazopakana nazo.


“Kuna watanzania pia wanaotembelea nchi za jirani kwa sababu za kiuchumi na kijamii.Hivyo uthibiti wa magonjwa ya kuambukiza si tu kwa ndani ya nchi bali hata kwa wale wanaosafiri kwenda nchi jirani kwa sababu maalumu.”amesistiza Bw.Lucas


Aidha. Mtafiti kutoka kitengo cha utafiti wa kitabibu,mafunzo na ushauri katika hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt.Sima Rugarabamu amesema kikao hiki kimefanyika wakati muhimu sana kwa nchi na dunia kwani itasaidia kuzuia magonjwa ya milipuko kama Mpox,mafua nakipindundu yanayoendela nchi jirani.


‘’Kazi tunayoifanya ni muhimu kwasababu itasaidia kuandaa mikakati  ya namna bora ya kufutilia na kudhibiti magonjwa  katika mipaka.”amesema Dkt.Rugarabamu


Pia Afisa mfawidhi kutokea Bandari ya Kigoma- ziwa Tanganyika Bw. Theodory.T.Rutahindurwa amesema uchambuzi huu utasaidia taarifa kuhusu mzunguko wa watu, makazi, wapi wanaposafiri na sababu ya safari hivyo itarahisisha kupanua wigo wa  huduma za afya zaidi ya mipaka rasmi ili kuzuia maambukizi.


“Taarifa hiyo inatarajiwa kutumiwa pia  na sekta mbalimbali zikiwemo afya, uhamiaji, usalama wa mipaka na mamlaka za serikali za mitaa, hatua itakayosaidia kuboresha mifumo ya tahadhari za mapema na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na milipuko ya magonjwa katika jamii za mipakani.” amesema Bw. Rutahindurwa

No comments